; Serengeti » Tanzania Tourist Board
 
Badilisha Lugha English Kiswahili

Serengeti

Maelezo kuhusu vivutio vya Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Serengeti ni hifadhi ya Taifa ambayo ni kubwa kuliko zote nchini ikiwa na eneo la kilometa za mraba za 14,763, na ina sifa za kimataifa. Kwa upande wa  kaskazani inapakana na Mbuga ya Masai Mara ya Kenya.

Hifadhi  hii ina mbuga za nyika zinazoendelea mpaka kwenye upeo wa macho huku ikipambwa hapa na pale na migunga. Hii inatoa picha halisi ya uasilia wa uzuri wa Afrika.  Vilima vingi vya mawe vilivyoko huko vinachangia kwa kiasi kikubwa umaarufu wa mfumo mzima wa ikologia.

Makundi makubwa  ya simba hupenda kujipumzisha kwenye majani marefu, tembo nao wakifaidi magome ya migunga, huku twiga na wanyamapori wengine wakishirikiana kuleta msisimko katika utajiri wa maliasili ya Afrika.

Watalii na wageni wengi toka nchi mbalimbali ulimwenguni wanahamasika kushuhudia makundi ya nyumbu yakiwa kwenye msimu wa misafara ya kuhama kati ya Serengeti na Masai Mara. Katika makundi haya, nyumbu kwa mamilioni, wakiwaongoza wanyama wengine, hufanya safari za kuelekea kaskazini na kisha kurudi kusini, kwa ajili ya kutafuta malisho. Vishindo vya wanyama hawa pamoja na wingu la vumbi jekundu, hasa nyakati za kiangazi, ni vitu vinavyoleta msisimko katika Hifadhi ya Serengeti. Misafara ya namna hii ni ya kila mwaka na ni moja ya Maajabu Saba ya Ulimwengu.

Mfumo mzima wa ekologia  ya Serengeti unategemea misafara ya wanyama hawa ambapo simba hujipatia mawindo yao huku tai na wanyama wala mizoga  wakisubiri mlo wao. Wakati huo huo mamba nao wanagoja wanyama wanaovuka mito wapate ridhiki yao.

Misafara hii haiihusishi Serengeti tu bali hupitia  pia kwenye mbuga za Maswa na Ikorongo upande wa kusini, Bonde la Ngorongoro na Mbuga za Masai Mara nchini Kenya. Umaarufu wa misafara ya nyumbu unafunika hata uzuri wa vivutio vingine katika Serengeti. Hata hivyo Hifadhi ya Serengeti ina vivutio vingine kama Seronera, Maswa, Mto Grumeti na Lobo.

Mbali nakutumia  magari, usafiri wa maputo ya hewa ya joto (hot air balloons) umekuwa wa kuvutia sana kwa wale wanaopenda kuangalia wanyama toka angani. Safari hizi mara nyingi huanza alfajiri ili kuwawezesha watalii kuona wanyamapori kwa ukaribu zaidi.

 

Mawasiliano

Contacting us by post Bodi ya Utalii
Jengo la IPS,Gorofa ya tatu
P.O.Box 2485
Dar-es-Salaam
Tanzania.
Contacting us by email info@tanzaniatourism.go.tz
Contacting us by telephone
General (+255) 022 2111244/5
Mkurugenzi Mwendeshaji 2110908
Masoko 2111345
Huduma za Kitalii 2128472
Utafiti 2111514
Contacting us by fax (255) 022 2116420

Je ulikuwa wajua?

Kuwa Dar-es-salaam ilikuwa ni kijiji cha uvuvi kilichojulikana kama ‘Mzizima’?