Iringa
Iringa, ulioko katika nyanda za juu kusini mwa Tanzania karibu na Makao Makuu ya Serikali, Dodoma, na mkoa maarufu kwa kilimo wa Morogoro, ni mji mdogo wa kuvutia na ni kituo muhimu kwa mazao yanayotokana na kilimo na bidhaa nyingine kwenye ukanda huo. Mitaa yake ni tulivu na soko lake kuu hunatoa fursa kwa mteja kupata bidhaa mbali mbali zenye mvuto wa utamaduni wa Mwafrika.
Mji wa Iringa unaangalia bondeni unakopita Mto Ruaha. Kwa mantiki hii hapa ni kituo kikuu cha watalii kuanza safari zao za kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Kihistoria, Iringa ilikuwa moja ya vituo vikuu vya kupinga utawala wa kikoloni, mpaka ikalazimu utawala wa Kijerumani kujenga ngome ili kupambana na Wahehe. Nje kidogo ya mji wa Iringa kuna jabali la Gangilonga mahali ambapo kiongozi wa Wahehe wakati ule, Chifu Mkwawa, alikutana na wafuasi wake kupanga mikakati ya kupambana na jeshi la Wajerumani.
Mji wa Iringa pia ulikuwa ni uwanja wa mapigano wakati wa Vita Vikuu ya Kwanza na ya Pili. Kama ukumbusho, makaburi ya wahanga wa vita yako nje kidogo ya mji.



Je ulikuwa wajua?


