; Unguja (Zanzibar) » Tanzania Tourist Board
 
Badilisha Lugha English Kiswahili

Unguja (Zanzibar)

Maelezo kuhusu vivutio vya Utalii katika Kisiwa cha Unguja (Zanzibar)

Unguja ni kisiwa kikuu ambacho, pamoja na Pemba vinaunda Zanzibar iliyoko katika Bahari ya Hindi, mashariki mwa Tanzania Bara. Kwa karne na karne, eneo la visiwa hivi lilijulikana kama Visiwa vya Marashi (Spice Islands) vilivyowavutia wageni wa kutoka nchi za mbali, hasa wafanya biashara ambao walipafanya kuwa ni  kiungo kikuu cha misafara kati ya nchi za nje na Bara la Afrika.

Kihistoria, Zanzibar ilikuwa chini ya himaya ya Waarabu wa Omani ambao kwa umaarufu wa visiwa hivi, watawala hao wakapafanya ndio makao makuu ya Serikali yao. Mikataba mikubwa ya kibiashara ilifanywa  na mataifa mengi ya Ulaya na Marekani. Uthibisho wa historia hii upo katika Mji Mkongwe wa Unguja (Stone Town) ambao sasa ni kivutio mahsusi cha utalii.

Kiutalii sehemu kadhaa za pwani ya Unguja kweli zina fukwe za kiwango cha kimataifa, lakini mvuto wake unatofautiana na mahali husika. Kwa mfano upande wa mashariki kuna upepo mwanana unaotokana na mawimbi. Wakati wa maji kupwa kunakuwepo na madimbwi ya hapa na pale yenye aina mbali mbali ya samaki wadogo wadogo wa kuvutia. Kaskazini ufukwe wake unatawaliwa na mawimbi makubwa lakini mchanga wake unavutia sana kwa ajili ya mapumziko. Kusini magharibi watalii wanapata fursa ya kuwaona na kuogelea na pombowe.

Sehemu kubwa ya pwani ya magharibi ni bandari ya Zanzibar ambapo fukwe yenye mvuto  iliyobaki ni Mangapwani hasa kutokana na historia kwamba njia hii ndiyo iliyokuwa inatumiwa kupitishia watumwa.

Nje kidogo ya Mji Mkongwe watalii wanaweza kupata burudani kwenye visiwa vidogo vya Snake, Prison na Grave pamoja na kutembelea mradi wa kuhifadhi matumbawe (CHICOP) katika kisiwa kidogo cha Chumbe.

Pwani ya kusini ya Zanzibar kuna Hifadhi ya Ghuba ya Menai inayotumika kuhifadhi na kuwaendeleza kasa ambao wamo hatarini kutoweka. Hifadhi hii inafikiwa kwa kupitia msitu wa Jozani ambao nao ni maarufu kwa mbega wekundu na aina nyingine za nyani pamoja na swala wadogo.

Mawasiliano

Contacting us by post Bodi ya Utalii
Jengo la IPS,Gorofa ya tatu
P.O.Box 2485
Dar-es-Salaam
Tanzania.
Contacting us by email info@tanzaniatourism.go.tz
Contacting us by telephone
General (+255) 022 2111244/5
Mkurugenzi Mwendeshaji 2110908
Masoko 2111345
Huduma za Kitalii 2128472
Utafiti 2111514
Contacting us by fax (255) 022 2116420

Je ulikuwa wajua?

Kuwa Dar-es-salaam ilikuwa ni kijiji cha uvuvi kilichojulikana kama ‘Mzizima’?